MTIZAMO WA KIKAFIRI JUU YA HISTORIA NA UDHAIFU WAKE

MTIZAMO WA KIKAFIRI JUU YA HISTORIA NA UDHAIFU WAKE

Assalaam alaykum.

Historia kwa waandishi wengi wa kileo hufasiriwa kama ni
kumbukumbu ya matendo ya mwanadamu. Matendo hayo yawe ni yenye kumwezesha mwanadamu kupata mahitaji yake muhimu kutoka kwenye maumbile ya asili (nature). Kwa makafiri mahitaji muhimu ya wanadamu ni chakula, nguo na makazi. Kwa hiyo matendo yote ya mwanadamu yana lengo moja tu; la kumpatia mahitaji muhimu ya maisha ambayo ni chakula, nguo na makazi.

Kwa mtizamo wao huo makafiri wameyahusisha matendo
yote ya mwanadamu na uzalishaji vitu au uzalishaji mali (Material Production). Kwa hiyo basi wakawa wanaiangalia historia katika ngazi mbili. Katika ngazi ya kwanza huiangalia historia kama somo lenye kuelezea mapambano ya mwanadamu dhidi ya mazingira yake. Mapambano ambayo ni ya lazima ili mwanadamu aweze kupiga hatua katika maendeleo.

Katika ngazi ya pili, makafiri huitazama historia kama somo
lenye kuonyesha vipi harakati za uzalishaji mali zinavyoathiri
uhusiano baina ya mtu na mtu.

Hii ni kutokana na imani yao kuwa mwanadamu ni mnyama
kama wanyama wengine. Na badiliko lolote litakalotokea kwa
binadamu aonekane tofauti na wanyama wengine, basi litakuwa ni zao la harakati zake dhidi ya maumbile (Nature). Kwa hiyo kwa makafiri kusoma historia ni muhimu kwa sababu huwasaidia kuelewa mabadiliko ya mahusiano kati ya mtu na mazingira yake na kati ya mtu na mtu. Na kwa njia hiyo wanaweza kufahamu hali ya mwanadamu iliyopita na ya sasa na hivyo kuweza kujiandaa ili kuukabili vyema wakati ujao.

Mtizamo huu wa makafiri katika kuiainisha historia una udhaifu mkubwa sana. Wao wamemtazama mwanaadamu na mazingira yake au kwa maneno mengine viumbe na mazingira yao na kumwachilia mbali Muumbaji wa vyote hivyo viwili.

Kama wangeingiza kipingele cha Muumba wangefaidika sana kwa sababu lengo la mwanadamu kuumbwa sio kuvaa nguo nzuri au kula sana au kuwa na nyumba nzuri. Bali lengu la kuumbwa mwanadamu ni kumpima na kumwandaa kwa ajili ya maisha ya baadaye huko akhera. Kama ukisahau kujiandaa na akhera ni hasara kubwa sana kwa sababu maisha ya hapa ni mafupi sana na maisha ya akhera ni ya milele. Hivyo utapoteza maisha ya milele kwa sababu ya starehe ya miaka sabini.

KISA CHA ISRA NA MIRAJ

KISA CHA ISRA NA MIRAJ

Aya 1: Israi Maana Ametakasika aliyempeleka usiku mja wake kutoka Msikiti Mtakatifu mpaka msikiti wa mbali ambaotumevibariki vilivyo kandoni mwake, ili tumuonyeshe baadhi ya ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.

Maana ya neno Israi katika lugha ya kiarabu ni kutembea usiku. Makusudio ya neno ‘mja wake’ hapa ni Muhammad (s.a.w.). Msikiti mtak- tifu ni ule ulioko Makka kwenye Al-ka’ba. Anasema mwenye Rawhul-lbayan na wengineo: “Riwaya iliyo sahihi zaidi ni kuwa safari ya Israi ilianzia kwenye nyumba ya Ummu Hani, dada yake Ali bin Abu Twalib.”

Msikiti wa mbali (Masjidul-Aqswa) ni hekalu la Nabii Suleiman. Umeitwa msikiti kwa sababu ni mahali pa kusujudu, kutokana na neno la Kiarabu masjid (msikiti) lenye maana ya mahali pa kusujudu. Na umeitwaMasjidul Aqswa (msikiti wa mbali), kwa sababu ya kuwa mbali na Makka. Msikiti huo umebarikiwa kandoni mwake kwa baraka za kidini, kwa vile ni nchi ya mitume na kwa baraka za kidunia kwa mito na miti. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuona.
Inawezekana ‘Yeye’ kuwa ni Mwenyezi Mungu kwa maana ya kuwa anamjua Mwenye kuamini na mwenye kukanusha tukio la Israi. Pia inawezekana kuwa ‘yeye’ hapa ni Muhammad (s.a.w.) kwa maana ya kuwa anajua ukuu na utukufu wa Mwenyezi Mungu.

Imesemekana kuwa Israi ilikuwa usiku wa kuamkia tarehe 27 Rajab (mfunguo kumi). Na pia imesemekana ilikuwa 17 Rabiul-awwal (mfunguo sita).

Ulama wengi wanalitumia neno israi kwa safari ya Mtume (s.a.w.) kutoka Masjidul-haram (Msikiti Mtukufu) ulioko Makka, hadi Masjidul-aqswa (Msikiti wa mbali) ulioko Baytul- muqaddas (Nyumba yenye kutakaswa).

Na wanalitumia neno Mi’raj (miraji) kwa safari ya kutoka Baytul-muqad- das hadi juu mbinguni. Wengine hawatofautishi baina ya maneno hayo mawili; wanatumia Miraji kwa kupanda mbinguni na Israi kwa kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas.

Wote wameafikiana kutokea tukio hili kutokana na nukuu za Qur’an na Hadith za Mtume. Lakini wametofautiana kuwa je, lilikuwa kwa roho tu bila ya mwili au kwa mwili na roho? Sisi tuko pamoja na wale wasemao lilikuwa kwa mwili na roho.

Wale wanaosema kuwa ilikuwa ni kwa mwili na roho wametoa dalili zifuatazo:
1. Israi ni jambo linaloingia akilini na dhahiri ya wahyi umelitolea dalili; pale aliposema Mwenyezi Mungu: “Aliempeleka usiku mja wake” na hakusema roho ya mja wake. Neno mja linatumika kwa roho na mwili; kama alivyosema Mwenye Mungu: “Je, unamuona yule ambaye anamkataza mja anaposwali?” (92: 10).

Misingi (usul) ya Uislamu iliyothibitishwa ni kuwa kila lililoelezwa na dhahiri ya wahyi na lisipingane na akili, basi ni lazima kuliamini. Kama Israi ingelikuwa ni kwa roho tu, kusingelikuwa na mshangao wowote, wala washirikina wasingeliharakisha kumfanya mwongo Muhammad. Kuna Hadith isemayo kuwa Ummu Hani alimwambia Mtume mtukufu (s.a.w.): “Usiwaambie watu wako hilo, nahofia watakufanya muongo,” lakini hakutilia maanani hofu ya Ummu Hani kwa kuona kuwa maadamu ni haki basi haina neno. Kwa hiyo akawatangazia watu wake aliyoyaona. Wakashangaa na wakampinga. Kama ingelikuwa ni kwa usingizi wasingelikuwa na mshangao huu.

2. Kwenda Israi kimwili na kiroho ni nembo ya kuwa kila mtu ni lazima ayafanyie kazi maisha yake ya kimwili na kiroho, sio upande mmoja tu.

3. Ni mashuhuri kuwa Mtume amesema: “Nilipelekwa usiku kwenye mnyama anayeitwa Buraq.” Ni wazi kwamba Israi ya kiroho peke yake haihitajii kupanda mnyama wala chombo chochote. Kwa mnasaba wa Buraq tutaashiria makala iliyo kwenye gazeti la Al-Jumhuriya la Misr, iliyoandikwa na Muhammad Fathi Ahmad, yenye kichwa cha maneno ‘Madhumuni ya kisayansi ya Israi na Miraji,’ Ninamnukuu: “Alipanda Mtume mtukufu mnyama anayeitwa Buraq. Kulingana na Hadith ni mnyama anayemzidi punda kwa kimo na yuko chini kidogo ya baghala. Hapo kuna somo kutoka kwa Mwenyezi Mungu tunapaswa tulitafutie maelezo Mwenyezi Mungu hashindwi kumchukua Mtume wake kutoka Makka hadi Baytul-Muqaddas bila ya nyenzo yoyote ambapo Mtume angeweza kujikuta tu yuko kwenye mlango wa Masjidul-aqswa.
Lakini Mwenyezi ambaye imetukuka hekima yake alipitisha kuwa kila kitu kiende kwa kanuni yake, bila ya mabadiliko wala mageuko. Safari hii iliyokata masafa marefu katika kasi ya kushangaza, inahimiza akili ianzishe nyenzo mpya ya kwenda masafa marefu katika muda mdogo. Kisha tujiulize, ni kitu gani katika ulimwengu kinakwenda kasi zaidi kulin- gana na utafiti wa elimu? Bila shaka jibu litakuja bila ya kusita kuwa ni mwangaza ambao unakwenda kwa kasi ya 300,000 km. kwa sekunde moja. Buraq aliyemtumia Mtume alitembea kwa kasi ya mwanga kwa sababu neno Buraq ni mnyambuliko wa nenoBarq lenye maana ya mwako kama wa umeme (flush). Kupitia majaribio ya kiakili katika uchunguzi wa anga za juu, binadamu ameweza kugundua siri nyingi na ameweza kwa nguvu ya elimu kupenya kutoka ardhini hadi kwenye ufalme wa mbingu. Lakini elimu ya maada pekee inamsahaulisha binadamu na muumba wake.

Tukio la Israi na Miraji linatupa somo kwamba maada na roho ziko sambamba. Kwa hiyo kwenda kwake kwenye utukufu wa juu kulikuwa ni kwa umbile la kibinadamu kutokana na maada na kuendeshwa kulikotokana na roho ya Muumba Mtukufu. Jibril akawa anachukua nafasi ya muelekezaji njia. Nasi hatuna kizuizi cha kumfanya ni nembo, kwa madaraka ya elimu, ambayo itatuongoza kwenye safari yetu katika maisha haya kuelekea kwa muumba wa ulimwengu”.

Ya kushangaza niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni kauli ya anayesema kuwa Israi ya Mtume (s.a.w.) ilikuwa kwa roho sio kwa mwili wake mtukufu kwa kutoa dalili ya hadith iliyopokewa kutoka kwa Aisha, kwamba mwili wa Mtume haukumwacha usiku ule. Na inajulikana kuwa wakati wa Israi, Aisha alikuwa mdogo, wala hakuwa ameolewa na Mtume (s.a.w.). Kwa hiyo Hadithi hiyo inajipinga yenyewe.

Masjidul-Haram Na Masjidul-Aqswa Masjidul-Aqswa unafanana na Masjidul-Haram katika mambo haya yafutayo:-

1. Yote iko upande wa mashariki.
2. Historia ya yote ni ya zamani; isipokuwa Masjidul-haram ni wa zamani zaidi na pia ni mtukufu zaidi. Kwa sababu ndiyo nyumba ya kwanza kujengwa kwa ajili ya ibada duniani: “Hakika nyumba ya kwanza waliyowekewa watu ni ile iliyoko Makka yenye kubarikiwa na mwongozo kwa viumbe. Mna humo ishara zilizo wazi: Mahali aliposimama Ibrahim. Na mwenye kuingia humo huwa katika amani; na ni haki ya Mwenyezi Mungu juu ya watu kuhiji nyumba hiyo kwa mwenye kuweza njia ya kuiendea. Juz. 4 (3:96–97).
3. Miji yote miwili, Makka ulio na Masjidul-haram na mji wa Quds ulio na Masjidul–Aqswa ilianzishwa na Waarabu au walishiriki kuianzisha. Makka ilijengwa na Ibrahim na mwanawe Ismail waliojenga Al-ka’aba: “Na tuliagana na Ibrahim na Ismail kuwa: Itakaseni nyumba yangu kwa ajili ya wale wenye kutufu na wenye kujitenga huko kwa ibada na wanaorukuu na kusujudu… Na Ibrahim alipoinua misingi ya ile Nyumba (Al-Kaaba) na Ismail (wakaomba): Ewe mola wetu! Tutakabalie; hakika wewe ndiye Msikizi, Mjuzi.” Juz. 1(2: 125, 127).

Inajulikana kuwa Ismail ndiye Mtume wa kwanza kuzungumza lugha ya Kiarabu ambayo haikuwa lugha ya baba yake. Maquraysh na waarabu wengineo wanatokana naye. Qur’an ilishuka kwa lugha yake. Quds nayo waliishi hapo wayabusi, kabila la waarabu wa Kanani. Walifika kwenye mlima maarufu unaojulikana kwa jina la Zayuni, mnamo mwaka wa 2500 (B.C.) kabla ya kuzaliwa Nabii Isa wakiongozwa na mzee wao aliyeitwa Salim Al-yabusi. Watu wa kabila hili ndio wa kwanza kuweka jiwe la kwanza la kujenga mji wa Quds ambao baadae ulikuwa ndio Qibla cha ulimwengu.
Baada ya Waislamu kuuteka mji wa Quds walijenga msikiti ulioitwa Masjid Umar, uliasisiwa na Umar bin A-khattwab na Masjid Qubbatusswakhra (msikiti wa kuba la mwamba) ulioasisiwa na Abdulmalik bin Marwan. Yote hiyo ilikuwa ndani ya haramu ya Quds. Waislamu walikuwa hawaruhusu asiyekuwa Mwislamu kukanyaga hapo.
4. Waislamu wanaitukuza misikiti yote miwili, ambapo mwanzo walikuwa wakiswali kwa kuelekea Masjiul-Aqswa kwa muda wa miaka 13 wakiwa Makka na miezi kadhaa Madina. Kuongezea safari ya Israi, inakuwa si jambo la ajabu kwa Waislamu kupafanya mahali hapo ni pa takatifu na ni pa pili baada ya Makka na Madina kwa utukufu, heshima na ulinzi.

Mapokezi mengi yanaeleza kuwa Mtume alimfunga Buraq hapo Baytul-Muqaddas. Mpaka sasa ukuta wa magharibi ya haram, mahali alipomfunga, unaitwa ukuta wa Buraq, pia mapokezi yanaeleza kuwa Mtume aliswali kwenye sehemu ya mwinuko katika hekalu la Nabii Suleiman, pamoja na Nabii Ibrahim, Musa na Isa akiwa yeye ndiye Imam.

Na kwamba yeye alitumia mwamba wa Ya’qub kuwa ndio kituo chake cha kupanda mbinguni. Ndio maana uharibifu wa Quds mnamo mwaka 1967 uliotekelezwa na wazayuni na wakoloni wa kimarekani na waingereza, ni maafa ya waislamu na wakiristo. Mkono mchafu ulichafua na kudharau sehemu takatifu za dini ya kiislamu na ya kikiristo. Usiku huo wa damu walikesha na ufuska; wakafanya sherehe za dansi na ulevi. Ajabu ya maajabu ni kwa Marekani na Uingereza kudai kuwa wao ni wahami wa dini na ni maadui wa ulahidi, wakati huo huo wakiwasaidia wazayuni ambao hawaamini misimamo yoyote, hawaheshimu maadili, hawaheshimu dini za wengine wala hawatambui haki yoyote katika haki za binadamu. Marekani na Uingerza zimeisaidia Israili, zikaipa mali na silaha na zikaiunga mkono kwenye Baraza la usalama na Umoja wa mataifa.

Zikaipongeza kwa kuingila sehemu takatifu za waislamu na wakiristo. Wameendelea na misimamo hii ulimwenguni pote. Sisi hatuna shaka kwamba iko siku itawafikia wakoloni na marafiki zao wazayuni kupitia mikononi mwa wanamapinduzi wapigania uhuru; kama ilivyowafikia hivi sasa wamarekani kutoka kwa wavietnam na kabla yake iliwafikia wazayuni kutoka kwa Nebuchadnezzar, Waroma, Mtume (s.a.w.) na Umar bin Al-khattwab.

Hivi sasa kila siku vyombo vya habari haviachi kutangaza habari za upinzani wa Palestina na kujitoa mhanga ambako kumeifanya Israil yote iishi kwenye jinamizi la hofu na woga.

Somo Katika Israi Qur’an hii ambayo tunaisoma ni masomo aliyompatia Muumbaji Mtume wake ili ayafikishe kwa watu wote.

MAPACHA WA ABDI-MANAF NA MAAFA YANAYOTUKUTA WAISLAMU

MAPACHA WA ABDI-MANAF NA MAAFA YANAYOTUKUTA WAISLAMU

Bwana Ibn Athir al-Jazari katika kitabu chake Tarikh al-Kamil anaandika kwamba Abdi-Manaf (Babu wa tatu wa Mtume wetu (s.a.w.w.)) alikuwa na watoto wawili Abdush-Shams na Hashim ambao wazizaliwa mapacha kwa hali kidole cha mmoja wao kiligandana na kipaji cha mwenziwe.

Walipofanyiwa kupasuliwa mahali pale paliposhikamana ikatoka damu nyingi. Wakasema watu: ‘hii ilionyesha kwamba baina ya ukoo wao patamwagika damu nyingi’. Aliposhika Bwana Hashim mahala pa baba yake Abdi-Manaf kuwa yeye mkubwa wa kabila, basi Ummayah mtoto wa Abdush-Shams akaona wivu juu yake, hivyo uadui baina ya watoto wa Hashim na Ummayah ukaanzia hapa.
Katika kitabu cha tafsir mashuhuri kiitwacho Durr al-Mansur cha Jalaluddin Suyuti imeandikwa hivi kwamba Ibn Jaree, Ibn Mundhir, Ibn Abi Hatim, Tabrani, Ibn Mardwaih na Hakim wamehadithia kwa njia sahihi mbali mbali kwamba Ali ameeleza tafsiri ya aya hii: ‘Alam-Tara Ilal-Ladhiyna Bad-Daluu Nia-Matal-Laahi Kufra”. (Je, hukuwaona wale waliobadilisha neema ya Mwenyeezi Mungu kwa kufru) (Sura Ibrahim, Aya 28) hivi, “Wale waliobadili dini ya Mwenyezi Mungu kwa kukufuru ni wana (watoto) wa Umayyah na watoto wa Mugheera, ambao ni wenye kupita kwa dhambi kuliko Quraesh wote.”

Ikumbukwe kuwa katika watoto wa Hashim waliyetajwa hapo awali ndimo alimopatikana Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlulbayt wake. Lakini watoto wa Umaya walitajwa kuwa ni waovu kuliko Quraish wote ndimo alimopatikana Uthuman bin Afan, Muawiyyah bin Abi Sufian, Yazid bin Muawiyyah na makhalifa wa uongo wengine waliowatawala waislamu kwa mkono wa chuma huku wakiwaua kwa halaiki kama walivyofanya Yazidi na Baba yake yaani Muawiyyah kwa kuendesha vita dhidi ya Ahlulbayt wa Mtume na kuwaua na kuwanajisi maelfu ya waislamu bila huruma wala chembe ya imani.

Tafadhali tujiepushe kuwafuata viongozi hao halifu kwa sababu mwisho wao haukuwa mwema bila shaka hata wafuasi wao hawatokuwa na mwisho mwema.

Uislamu sahihi ni kumfuata Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlulbayt wake.

MATENDO MATUKUFU KWA MUISLAMU {V}

MATENDO MATUKUFU KWA MUISLAMU {V}
{1}Kusameheana:
Mwenyezi Mungu amesema: “Na mkiwasamehe na kupuuza yaliyopita na kuyafuta kabisa katika nyoyo zenu {basi Mwenyezi Mungu} atafurahi kwani Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mwingi wa rehema.” {Qur’an, Sura ya 64, aya ya 14}.

 

Hivyo waislamu tunatakiwa tuwe wepesi wa kuwasamehe waliotukosea, hasa pale wanapotuomba msamaha tusithubutu kugoma kuwasamehe, vingine nasi hatutosamehewa na Allah (s.w).
{2}Kukidhi haja za watu:
Mtukufu Mtume {s.a.w.w.} amesema: “Mwenye kukidhi haja ya nduguye mwenye kuamini {Muislamu} basi kama amefanya ibada ya Mwenyezi Mungu maisha yake.”
Waislamu tunahitaji kutoa misaada kwa wahitaji wote bila kujali dini wale upendeleo, japokuwa waislamu wanatakiwa wawekewe mpango maalumu wa kuwainua kiuchumi na kijamii.

 

{3}Kufanya usawa kwa kila kitu:
Mtukufu Mtume {s.a.w.w.} amesema: “Unachopendelea kwa ajili ya nafsi yako, wapendelee wenzio pia. Fanya usawa kati ya wake wako kama unao wengi na kati ya wanao, wala usipendelee kabisa.”
Mwenyezi Mungu amesema: Lawama iko juu ya wale wanao dhulumu watu na wakawafanyia jeuri katika ardhi pasipo haki. hao ndio watakao pata adhabu. {Qur’an, Sura ya 42 aya ya 42}

MFUMO WA JUA (SOLAR SYSTEM)

Kwa mujibu wa taaluma ya sayansi, Dunia (earth) na sayari nyingine zinazozunguka jua, hufanya ulimwengu (universe) ambao kwa vipimo vyetu vya kibinaadamu ni mkubwa mno.

Dunia (earth) yetu hii ipo umbali wa kiasi cha maili 93 Milioni kutoka kwenye jua. Umbali huu ni mkubwa sana kwa mwanaadamu, lakini ni mdogo sana ukilinganishwa na umbali unaolitenganisha jua na sayari iliyo mbali kuliko zote katika “Solar System” yetu hii, Pluto. Umbali baina ya jua na Pluto ni mara 40 zaidi ya umbali kati ya jua na dunia. Yaani kiasi cha maili 3720 Milioni. Pamoja na kuwa mwanga wa jua husafiri kwa mwendo wa kasi sana – mwendo wa maili 186,000 kwa sekunde, lakini huchukua takriban saa 6 kwa mwanga huo kufikia Pluto.

Dunia ina umbo la duara dufu, yaani duara isiyokamilifu mfano wa chungwa, kwa maana kwamba umbali kutoka ncha ya kaskazini kwenda ncha ya kusini ni mfupi zaidi ya umbali kutoka mashariki mpaka magharibi kwa katikati ya dunia.

Dunia hulizunguka jua katika mzunguko ambao waingereza huuita revolution kwa muda wa mwaka mmoja. Yaani kila mwaka mmoja dunia hukamilisha mzunguko mmoja wa kulizunguka jua. Mzunguko huu ndio huzaa majira mbali mbali ya mwaka, yaani masika na kiangazi kwa uchache.

Dunia pia hujizungusha yenyewe katika mhimili wake. Mzunguko huu waingereza huuita rotation na huichukua dunia siku moja (saa 24) kukamilisha mzunguko wake mmoja wa kujizungusha kwenye mhimili wake. Hatima ya mzunguko huu ni kutengeneza usiku na mchana, kutokana na upande mmoja kuangaziwa na miale ya jua na upande mwingine kuwa gizani.

Huu ndio ulimwengu unaomzunguka mwanadamu kama unavyotambulika na wanasayansi.

UCHAMBUZI WA HOTUBA YA SHEIKH UWESU KATIKA MAZISHI YA DOCTOR KABOUR.

UCHAMBUZI  WA HOTUBA YA SHEIKH UWESU KATIKA MAZISHI YA DOCTOR KABOUR.

Wiki hii tulimpoteza kiongozi maarufu wa mkoa wa Kigoma, na Tanzania kwa ujumla, hususan kwa upande wa CHADEMA NA C.C.M.

Dr Kabour alikuwa mbunge wa kwanza wa upinzani Tanzania nzima kuingia bungeni kwa tiketi ya chama cha upinzani (CHADEMA). Yeye aliingia bungeni kabla ya uchaguzi mkuu uliohusisha vyama vingi vya siasa mwaka 1995. Hii ilitokana na uchaguzi mdogo uliofanyika Manispaa ya kigoma Ujiji baada ya kumpoteza mbunge wake wa kipindi hicho, marehemu Rajabu Mbano.

Dr. Kabour aliwahi kuwa makamu mwenyekiti wa CHADEMA taifa,  mbunge wa Afrika na mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kigoma. Alifariki wiki hii alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya taifa Muhimbili na kusafirishwa hadi kigoma na kuzikwa Ujiji siku ya Ijumaa iliyopita.

Tunamwomba Allah amsamehe, na kumwingiza katika rehema zake. (Sote tuitike Ameen).

 

Sheikh Uwezo Khalifan Kiumbe anasema, kumekuwepo na mijadala katika vijiwe, hususani vya kahawa kujadili uhalali wa sisi kumsafirisha Marehemu Kabour kutoka Dar Es Salaam mpaka Kigoma umbali wa zaidi ya kilometa elfu moja, wakati Mtume alituagiza Mtu azikwe mahali alipofia.

 

Akilitetea tendo lao hilo anasema kuwa walimsafirisha marehemu kwa sababu huo ndio ulikuwa wosia wake, yaani azikwe Ujiji, na kaburi lake lijengewe baada ya siku saba tokea kuzikwa.

 

Akaendelea kusema kuwa katika Uislamu wosia ni muhimu uzingatiwe. Na hilo sio geni kutekeleza wosia ulioachwa na Marehemu. Kisha akatoa mfano wa wosia waliowahi kuutekelezwa na masahaba wa Mtume (s.a.w).

 

Akasema kuwa Bibi Fatuma bint Rasulillah (s.a.w) alikufa akiwa hawaridhii mabwana wawili Abubakar na Omar. Fatuma ndio mtoto pekee aliyeachwa na Mtume pindi alipofariki. Ieleweke kuwa Mtume anasema kuwa Fatuma (a.s) ni mwanamke wa kwanza kuingia peponi. Hivyo jambo alilofanya haliwezi kuwa nje ya Uislamu.

 

Baada ya baba yake (Mtume) kufariki, na Abubakar kuchukua ukhalifa, alikwenda kwa Abubakar kudai mirathi yake. Abubakar akadai kuwa alimsikia Mtume akisema kuwa mitume hawarithiwi. Ikabidi Fatuma akose mirathi yake na hapo akamchukia sana Abubakar.

 

Siku chache baadaye bibi huyu akafariki na kuacha wosia kuwa mabwana wawili Abubakar na Umar wasihudhurie mazishi yake. Hili lilitekelezwa na mabwana hao hawakuhudhuria mazishi yake. Huu ni mfano wa utekelezaji wa wosia wa marehemu tena uliofanywa na watu wema.

 

Kwa bahati mbaya hakueleza sababu za bibi huyu mtukufu kumchukia Omar. Lakini kwa wachunguzi wa mambo wanafahamu. Ukweli ni kuwa ukhalifa wa Abubakar ulitokana na Omar kuwalazimisha watu wamtii Abubakar, kiasi kwamba alikwenda nyumbani kwa bibi huyu mara nyingi na kuwalazimisha waislamu waliokuwa wakijua kuwa khalifa wa kwanza ni imam Ally (a.s) wabadili misimamo na hivyo kumtii Abubakar kama khalifa wa kwanza.

 

Katika pilika pilika hizi, alifikia mahala kupiga ngumi mlango wa bibi huyu na yeye akiwa nyuma yake, hapo mlango ukampiga tumboni na kupelekea kupoteza ujauzito aliokuwa nao, ndipo akaugulia kipigo hiki na miezi miwili baadaye akafariki dunia. Hivyo alimchukia Omar kwa sababu ndiye aliyekuwa sababu ya kifo chake.

 

Ikumbukwe kuwa Uwesu huyu ndiye yule yule aliyesimama majukwaani na kudai kuwa mashia ni makafiri. Tulipomuuliza ukafiri wetu akasema kuwa tunawatukana maswahaba. Tulipomwambia tukisemacho ni historia iliyomo katika vitabu vya Ahlul Sunnah alidai kuwa ni mashia ndio waliozipachika historia hizo katika vitabu vyao.  

Lakini leo anakuja na maelezo yale yale ambayo yanaponukuliwa na Mashia, wao huchachamaa na kudai kuwa mashia wanawatukana masahaba.

 

Hoja zangu ni hizi:

  1. Nani alikuwa kwenye haki kati ya bibi Fatuma na Abubakar katika suala la mirathi?
  2. Je mtu mtakatifu kama Fatuma anaweza kwenda kudai mali zisizokuwa halali yake? Na bado awe mtu wa peponi?
  3. Qur’an inasema kila mtu anarithiwa, je mitume hawakuwa watu?
  4. Qur’an inasema kuwa Seleman alimrithi Daudi, je Daudi hakuwa mtume? Mbona alirithiwa na Seleman?
  5. Je aliyedhulumu na aliyedhulumiwa, wote kwa pamoja wamo katika haki? Fikiri kiundani.
  6. Wakati akitutukana mashia kwamba hoja zetu zinawatukana maswahaba, je Uwesu hakuwa amevisoma vitabu vya historia na kuuona ukweli huo? Je sasa ndio ameuona ukweli? Kama ameujua ukweli hatutegemea achukie pale tutakapo hadithia historia za masahaba waovu na madhalimu.

 

  1. Au alikuwa akiujua lakini alikuwa akiuficha ukweli? Kama alikuwa akiuficha ukweli basi atakuwa ni mnafiki na wafuasi wake pia ni wanafiki.